OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ
BARAZA LA JIJI LA ZANZIBAR

HISTORIA YA JIJI LA ZANZIBAR
Usimamizi wa Jiji la Zanzibar ulianza tokea wakati wa ukoloni ambapo mnamo mwaka 1944 ilianzishwa “Zanzibar Town Board” kwa Sheria Nam. 6/1944 na baadae kurekebishwa kwa Sheria Nam. 24 ya 1949 iloyoanzisha “Stone Town Council” kwa ajili ya kutoa huduma katika Mji Mkongwe. Aidha, kwa upande wa nje ya Mji Mkongwe usimaizii ulifanywa na Chombo kilichoitwa “Ng’ambo Municipal Council”. Vyombo hivyo vilidumu hadi Machi 1950 ilipoanzishwa “Joint Township Council” kwa kuunganishwa kwa “Stone Town Council” na “Ng’ambo Municipal Council” ili kutoa huduma kwa mji wote wa Zanzibar. Majukumu makuu ya vyombo hivyo yalikuwa ni pamoja na kusimamia uendelezaji wa ujenzi, miundombinu na huduma za jamii. Kazi za vyombo hivyo zilijumuisha utoaji wa idhini, ruhusa na kudhibiti uendelezaji ujenzi katika maeneo yake husika.
Mnamo mwaka1969, utaratibu wa usimamizi wa miji ulihamishiwa katika Serikali za Mitaa ambapo Baraza la Mji (Zanzibar Town Council) lilifanya kazi hiyo ndani ya mipaka ya Wilaya ya Mjini inayopakana na Wilaya ya Magharibi kwa upande wa Mashariki.
Mnamo mwaka 1986, Serikali ililipandisha hadhi Baraza la Miji wa Zanzibar na kuwa Manispaa ya Mji wa Zanzibar ili kuweza kusimamia shughuli za uendelezaji wa mji katika Wilaya Mjini pamoja baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Magharibi yaliyofanyiwa Mpango wa Matumizi ya Ardhi kwa mujibu wa Mpango Mkuu wa Matumizi ya Ardhi wa mwaka 1982 wa Mji wa Zanzibar.
Mnamo mwakwa 1995, zilitungwa Sheria Nam. 3/1995 na Nam 4/1995 na kupekelekea kuiunda upya Manispa ya Mji wa Zanzibar (Zanzibar Municipal Council) kwa kuzingatia mipaka ya Wilaya ya Mjini tu na kuundwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi ili kuweza kusimamia masuala ya utoaji wa huduma za jamii, usimamizi wa uendelezaji miji na usafi katika Wilaya ya Magharibi. Kuanzishwa kwa Halmashauri hiyo kulichangiwa na kuwepo kwa maeneo (neighbourhoods) ya Mpango Mkuu wa Matumizi ya Ardhi ya Mji wa Zanzibar uliotambulikana kwa jina Zanzibar Master Plan ya mwaka 1982 ndani ya Wilaya ya Magharibi ambayo yalihitaji usimamizi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa iliomo katika eneo (Wilaya) husika. Aidha, Wilaya ya Magharibi tayari ilikuwa na baadhi ya maeneo yaliyokuwa na hadhi ya kimji (urban characteristics) yaliyokuwa yakikua kwa kasi na kuhitaji usimamizi mzuri na wa wakaribu.
Katika mwaka 2012, Serikali ilitunga Sera na Sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa Nam 07/2014 iliyopekelea kuanzishwa kwa Manispaa za Magharibi “A” na Manispaa ya Magharibi ”B” mnamo mwaka 2016. Hatua hiyo ilitanguliwa na kuongezeka kwa Idadi ya watu, kupanuka na kuimarika kwa makaazi na kukua kwa shughuli za kiuchumi na kijamii katika Wilaya ya Magharibi ambako kulipelekea Serikali kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi na kuanzisha Manispaa ya Magharibi “A” na Manispaa ya Magharibi “B”. Sambamba na hatua hiyo, mnamo mwezi wa Agosti 2019 Serikali kwa Sheria hiyo hiyo Nam 07/2014 ilianzisha Baraza la Jiji la Zanzibar ili pamoja na mambo mengine kusimamia Mabaraza ya Manispaa za Jiji ziliomo katika Mkoa wa Mjini Magharibi ili kuimarisha utendaji wake kimkoa